USICHOKIJUA KUHUSU SALIM KIKEKE WA BBC
NDUGU mpenzi msomaji au mfuatiliaji wa story hii ya sallimu kikeke wa BBC na leo tunawaletea sehemu ya pili ya story hii na hapa ndipo tulipoishia.
Kuingia utangazaji
Mara baada ya kuona matumaini
yakififia kupitia taaluma yake ya kilimo, Kikeke aliamua kubadilisha ukurasa wa
maisha baada ya kupiga hodi katika ofisi za kituo cha TV cha CTN ambacho
kilikuwa na redio wakati huo ikijulikana kama Classic FM ambayo kwa sasa ni
Magic FM.
Sababu, nia na ujasiri wa kuchukua
uamuzi huo, haikutokea kama ajali, bali ilitokana na ushawishi aliokuwa
ameupata kutoka kwa mama yake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa.
“Mama yangu alikuwa wa kwanza
kunijengea uwezo wa kuingia katika utangazaji, alikuwa anapenda sana kusikiliza
habari za redioni na alinishawishi kufuatilia kila habari iliyokuwa inaendelea
duniani, nikawa na uwezo wa kutamka maneno vizuri na kusoma habari,” anasema
Kikeke.
Ilikuwa ni mwishoni mwa 1997, Kikeke
alifika katika ofisi za kituo cha kurusha matangazo cha CTN. “Kwa sasa
wanaita Magic FM, walikuwa wanafungua kituo kipya cha Classic FM hivyo niliomba
kufanya kazi bure, nikapewa kipindi cha kucheza miziki ya Kiingereza,” anasema
Kikeke.
Jambo la kujifunza
Jambo la kujifunza hapa ni kwamba
wakati mwingine katika kusaka ajira, kubali kufanya kazi bila ya malipo,
onyesha jitihada zako, huenda ikawa ni njia nzuri ya kuajiriwa katika maeneo
mbalimbali yakiwemo yale ambayo huenda mtu amekwenda kwa ajili ya masomo kwa
vitendo.
Njia sahihi ya kukaa katika ajira usiyo na ujuzi nayo
Anasema baada ya kupata uhakika wa
kuendelea na kazi hiyo, Januari mwaka 1998, Kikeke aliamua kwenda kusoma kozi
fupi ya Utangazaji habari katika chuo cha uandishi wa habari cha ‘Tanzania
School of Journalism (TSJ)’.
”Pale nilisoma cheti kwa miezi
mitatu na kurudi tena kazini, nikaanza kusoma habari za kiingereza na Kiswahili
wakati mwingine nilikuwa naenda kutafuta habari,” anasema Kikeke.
Mafanikio yameanza kuja, lakini
ghafla anafukuzwa kazi!
“Hata hivyo mwezi mmoja
baadaye wakanifukuza kazi kwa sababu ambazo nisingependa kufafanua
zaidi,” anasema.
Wakati mwingine hata baya lina uzuri
wake
Kikeke baada ya kufukuzwa kazi,
hakuishia kulia mtaani, badala yake alianzisha mkakati wa kusaka ajira tena
kwenye taasisi yenye hadhi ya juu zaidi, Radio Tanzania (RTD) ambayo sasa ni
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), hiyo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1998.
”Kwa kipindi hicho Abdul Ngarawa
alikuwa mkurugenzi wa RTD, nikapelekwa idhaa ya Kiingereza, ‘English
Service’, na kuandaa vipindi vya muziki kila siku kuanzia saa 12:00 jioni mpaka
saa 6:00 usiku,” anasema Kikeke na kufafanua kuwa alikuwa akifanya kazi kwa
muda ‘part-time.
Alianza kupangiwa vipindi vya
kutangaza baada ya kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja. “Baadaye nikapewa
kipindi cha Mwelekeo kilichoanzishwa wakati wa maandalizi ya kuelekea Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2000, nilikuwa mtangazaji wa mwanzoni kabisa katika kipindi
hicho,” anasema Kikeke.
Katika kipindi hicho, Radio Tanzania
walianzisha kituo cha matangazo cha FM, kiitwacho PRT kikitoa matangazo kwa
lugha ya Kiingereza.
RTD na Kituo cha PRT ndizo kwa sasa
zinafahamika kama TBC na TBC1. “Mimi nikaondoka pale na kurudi tena CTN,” anasema.
Kurudi CTN
Baada ya kurudi katika kituo hicho,
Kikeke alifanikiwa kupata nafasi ya kusoma habari kwenye TV mpaka mwezi Agosti
wakati kampuni hiyo ilipouzwa na kuwa chini ya kituo cha Channel Ten na DTV.
Baadae alihamia ITV.
Kuingia ITV/Radio One
Baada ya hapo alifanikiwa kuandika
barua ya maombi ya kazi katika Kituo cha Radio One.
“Kwa wakati huo Charles Hilary ndiye
alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Radio One, akaniomba nimpatie mfano (Demo) ya
kipindi chochote nilichowahi kufanya, kwa bahati mbaya sikuwa na ya radio ila
nikawa na ya TV”, anasema Kikeke.
Anaongeza kuwa hali hiyo ikamfanya
abadilishe mlango wa kutoka Redio One na kuingia ITV. “Charles Hilary
akaipeleka ile demo upande wa televisheni ya ITV, kulikuwa na Betty Mkwasa na
Joyce Mhaville, wakaipenda kazi yangu na kuagiza niripoti pale kazini,”
anasema.
Kikeke alipangiwa jukumu la
utangazaji wa vipindi vya taarifa za habari kila siku na habari za ‘Jiji Letu’
hata hivyo mambo yalibadilika kwa muda mfupi pale ofisini.
Safari ya BBC
Radio One walikuwa ni Redio
washirika wa BBC hivyo walikuwa na mkataba wa kuchukua mtangazaji mmoja kila
mwaka na kumpeleka kufanya kazi makao makuu ya BBC kwa muda wa miezi kadhaa.
Anasema Mwezi Mei 2003 nikafaulu
majaribio ya kuingia BBC, ambako anaendelea hadi leo.
Familia yake
Kikeke ni mtoto wa pili kati ya
watoto watatu. Ni baba wa mtoto mmoja ambaye anasoma darasa la saba nchini.
“Huku London ninaishi peke yangu,” anasema.
tumefikia mwisho wa story hii. source. mwananchi.co.tz
tumefikia mwisho wa story hii. source. mwananchi.co.tz
USICHOKIJUA KUHUSU SALIM KIKEKE WA BBC
Reviewed by mudy mandai
on
12/14/2015 01:03:00 PM
Rating:
No comments: