UKAWA YAPATA PIGO KUBWA..KIONGOZI WAO KUUGUA GHAFLA
Mabere Marando
Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando,amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, huku hali yake ikielezwa kuwa tete baada ya kuugua ghafla juzi nyumbani kwake.Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu.
Mmoja wa wauguzi wa zamu katika kitengo hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa madai siyo msemaji wa mgonjwa huyo wala hospitali, alisema Marando alifikishwa hospitalini hapo juzi akiwa na hali mbaya.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa watu wa karibu na Marando hali yake inaleta matumaini ikilinganishwa na alivyofikishwa hospitalini hapo juzi.
Alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya hawawezi kuruhusu waandishi wa habari kuchukua taarifa yoyote na kwamba hata mke wake amekataa kutoa taarifa za mume wake hadi hapo atakapopona.
“Hata mkienda hamuwezi kuongea naye chochote na tangu asubuhi ukimuuliza kitu anakuangalia tu na anapotaka kuzungumza anabaki anaguna, kwa hiyo kwa hali yake hawezi kuzungumza,” alisema muuguzi huyo.
Alisema wanamatumaini hali ya Marando itakuwa nzuri zaidi baada ya siku mbili kwani kuna dawa wamempatia ambazo zinahitaji apumzike.
“Unajua hawa wanasiasa wanakosa muda wa kupumzika kutokana na kazi zao na hata hapa tunamuona anahamu ya kuzungumza chochote lakini hawezi kutokana na hali yake ndiyo maana tunataka apumzike zaidi,” alisema.
Naye mmoja wa ndugu wa Marando ambaye pia hakutaka kujitambulisha jina lake, alisema mwanasheria huyo aliugua gafla akiwa nyumbani kwake juzi usiku.
“Jana mchana hadi jioni (juzi) nilikuwa naye lakini nilishangaa kupigiwa simu usiku kuelezwa kuwa aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na hata hivyo hatujaweza kuzungumza naye zaidi ya kupewa taarifa za hali yake na mke wake,” alisema ndugu huyo.
Alisema tangu wamempeleka hospitalini hapo bado hali yake ni mbaya ingawa anaendelea na matibabu.
Sababu za ndugu hao kuishia nje zilielezwa kuwa ni kutokana na hali ya Marando kutohitaji usumbufu wa watu kuingia wodini.
Miongoni mwa ndugu waliokuwa hospitalini hapo ni mama mzazi wa Marando ambaye alikuwa amekaa nje akisubiri taarifa ya hali ya mwanaye.
Mtu mwingine wa karibu na Marando ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema, aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa hospitali ya kwanza ambayo hata hivyo hakutaja jina na baada ya kumpatia huduma ya kwanza walisema hawawezi kumtibu na hivyo kuhamishiwa Hospitali ya Muhimbili.
“Hapa hospitali walimleta usiku akaanza kupatiwa matibabu na hali yake ilikuwa mbaya lakini baada ya kupatiwa matibabu inaendelea vizuri kidogo,” alisema.
Kwa upande wa mke wake ambaye pia hakutaka kujitambulish jina alisema kuwa, hawezi kuzungumzia hali ya mumewe bila ridhaa yake.
Mkewe huyo alitoka wodini majira ya saa 11:00 jioni na kuwapatia ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamesimama nje ya jengo hilo taarifa ya hali ya mumewe.
Alisema ni kweli mumewe ni mgonjwa lakini taarifa ugonjwa wake ataitoa mwenyewe.
“Ni kweli mume wangu ni mgonjwa lakini siwezi kumzungumzia bila kibali chake na kuna waandishi wengine wamekuja sijawapa taarifa. Huyu ni mwanasiasa na mnafahamiana, akipona tu atazungumza mwenyewe kila kitu,” alisema na kuondoka eneo hilo.
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Steven, alithibitisha kupokelewa Marando hospitalini hapo juzi saa 4:00 usiku.
“Ni kweli Marando kalazwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anapata matibabu lakini taarifa kamili ya ugonjwa wake unaweza kuipata kwa mwenyewe wodini au kwa ndugu,” alisema Steven.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hana taarifa ya kuugua kwa Marando.
sos; the choice
UKAWA YAPATA PIGO KUBWA..KIONGOZI WAO KUUGUA GHAFLA
Reviewed by habarinamatukioyakijamii.brogspot.com
on
9/08/2015 03:14:00 PM
Rating: