BREAKING NEWS

recent

BREAKING NEWZZZ; KWA UOZO HUU TRA NA TPA, MAHAKAMA YA MAFISADI IJE FASTA.

pombe
ZIARA za kushtukiza za Rais John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika taasisi mbili tu za TRA na TPA zimewaonesha Watanzania jinsi ambavyo baadhi ya watumishi wa serikali wanavyotumia ofisi za umma kujiingizia vipato vya mabilioni ya shilingi kwa njia haramu.

Kama mtu mmoja ameweza kukutwa akimiliki nyumba zaidi ya sabini ni wazi kuwa wapo maelfu ya watumishi hao wenye majumba kibao, miradi, kampuni na shughuli nyingine nyingi za kiuchumi zinazotokana na mapato ambayo yangeingia serikalini.

Lakini siyo tu kuona jinsi watumishi hao wanavyotumia ofisi na mamlaka waliyopewa na serikali wakijinufaisha wenyewe, bali pia jinsi wanavyopuuza kuona wananchi wakifanyiwa vitendo visivyopendeza, ikiwa ni pamoja na kudhulumiwa, kuibiwa au hata kunyanyaswa na watu au taasisi ambazo zilipaswa kushughulikiwa.

Tunaposikia serikali ikiwa kali kuhusu matumizi ya ovyo ya pesa za umma, ubadhirifu na ukwepaji kodi, tunapata faraja kwamba sasa wakati wa watu kuogopa matendo hayo umefika.

Kitu kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya taifa hili ni watumishi wa umma walio katika sekta mbalimbali, ambao pengine kwa kuwaangalia viongozi wao wa juu, wanatumia muda mwingi zaidi kujifikiria wenyewe kuliko majukumu waliyopewa kuyatimiza.

Ni aibu waziri, naibu, katibu mkuu, wakurugenzi na vigogo wengine wa wizara kupishana angani wakienda Ulaya, badala ya kwenda vijijini waliko wananchi. Kama alivyosisitiza Rais Magufuli, viongozi hawa wanapaswa sasa kuhamishia safari zao kwenye makazi ya watu ili wawaone wanavyoishi.

Lakini wakati tunasisitiza umuhimu wa viongozi hao kwenda huko vijijini, suala la ubadhirifu wa mali ya umma limekuwa ni jambo la kawaida kabisa katika nchi hii. Kila mtu mwenye dhamana katika eneo lake anatumia fursa kujineemesha.

Watumishi hawa lazima wabanwe, siyo tu kutumia vizuri mapato ya serikali, lakini pia kukomesha mianya yote inayowafanya kujipatia fedha isivyo halali, iwe kwa udanganyifu wa malipo au hata kujitengenezea mazingira ya rushwa kupitia utendaji wao.

Sheria ya maadili ya viongozi wa umma ifuatwe na kuzingatiwa ili mtumishi wa serikali ajaze fomu akitaja mali zake siku anaanza kazi na pia siku ya kuacha au kustaafu. Tuondoe utamaduni huu wa kuzalisha mamilionea wanaotokana na utumishi wao kwa umma.

Ni vipi mtumishi wa serikali anajenga jumba la mabilioni halafu hatuoni watu wa TAKUKURU wakimpekua ili kujiridhisha? Mabilioni haya yanayokwenda kwa mtu mmoja yangeweza kuwasaidia wengi katika hospitali, shule na hata ujenzi wa miundombinu imara kama barabara, mabomba ya maji na hata nyaya za umeme.

Kama serikali itakunjua makucha, tutaweza kurejesha fedha hizo zinazoibwa na hawa watumishi, achilia mbali wanazowasaidia wafanyabiashara kutolipa kodi, ushuru na malipo mengine stahiki.

Hii ikifanyika, nidhamu ya kazi itakuwepo kwa sababu kila mmoja atatambua kuwa jukumu lake katika ofisi ya umma ni kumtumikia Mtanzania badala ya kuzitumia kujinufaisha na wakati huohuo kuwadharau na kuwakejeli wananchi.

Ile mahakama ya ufisadi ianzishwe mara moja na adhabu kali zitolewe ili kukomesha kabisa tabia hii. Kama watu wanataka utajiri wajihusishe na biashara, maana huwezi kuwa na ndoto mbili kwa wakati mmoja na kila upande ukapata unachostahili.

Wasaidizi wa rais, kuanzia mawaziri wawe wawakilishi wa kasi hii ya Magufuli. Tunataka kuona kero za wananchi zikipungua ili tufurahie utofauti wa viongozi waliopita na hawa wa awamu ya tano.

Hatutaki porojo za kukua kwa uchumi katika makaratasi wakati mifuko ya wananchi ikizidi kukauka kila kukicha.
BREAKING NEWZZZ; KWA UOZO HUU TRA NA TPA, MAHAKAMA YA MAFISADI IJE FASTA. Reviewed by habarinamatukioyakijamii.brogspot.com on 12/18/2015 09:46:00 AM Rating: 5

No comments:

All Rights Reserved by habartz © 2014 - 2015
Designed by JOJOThemes

Contact Form

Name

Email *

Message *

HABARI NA MATUKIO YA KIJAMIII. Powered by Blogger.