DR MAGUFULI SIKU YA KWANZA IKULU
BAADA ya kuapishwa rasmi jana katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, leo ndiyo siku ya kwanza kwa Rais John Pombe Magufuli kuanza kazi rasmi akiwa Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Magufuli aliapishwa jana katika tukio lililoshuhudiwa na mamilioni ya watu mbalimbali duniani kote, kwani hafla hiyo ilirushwa na vituo vingi vya televisheni vya ndani na nje ya nchi, huku baadhi ya viongozi na watu wengine mashuhuri duniani wakiwemo.
Mamia ya wakazi wa Dar es Salaam waliozungumza na gazeti hili, walisema siku ya kwanza ya kiongozi huyo inatoa dalili ya kutokea kwa mabadiliko makubwa ya nchi kiutendaji, kwani wana matumaini makubwa ya kutimizwa kwa ahadi alizoahidi wakati wa kampeni zake za urais.
“Tuna matumaini makubwa sana na Magufuli kwa sababu historia ya utendaji wake inaeleweka. Ninajua viongozi wazembe, wabadhirifu na wababaishaji hivi sasa matumbo yako moto, wanajua huyu jamaa hana mchezo, tunaisubiri Tanzania mpya ya Magufuli,” alisema Johny Fammy, muuzaji wa vinyago nje ya nchi, aliyezungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake waliopatikana Mwenge kijijini.
Kazi ya kwanza ya rais Magufuli itakuwa ni kuteua jina la mbunge mmoja wa kuchaguliwa ili kushika nafasi ya waziri mkuu, atakayeshika usukani unaoachwa na Mizengo Pinda, aliyedumu katika nafasi hiyo tangu Februari 2008, alipomrithi Edward Ngoyai Lowassa. Jina hilo itabidi kuidhinishwa na Bunge ambalo litaanza vikao vyake wakati wowote kuanzia sasa.
DR MAGUFULI SIKU YA KWANZA IKULU
Reviewed by mudy mandai
on
11/06/2015 01:32:00 PM
Rating:
No comments: