LOWASSA ADAIWA KUKODI MAKOMANDOO WA ISRAEL
Lowassa adaiwa kukodi
makomandoo wa Israel
*Yadaiwa ni kwa ajili ya kumpa ulinzi
*Mkurugenzi Usalama wa Taifa ahusishwa
*IGP Mangu ashtushwa, Chadema yang'aka
WAKATI Jeshi la Polisi likipiga marufuku vyama vya siasa kuacha kutumia vikundi vya ulinzi, mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa anadaiwa kuipa zabuni kampuni kutoka Israel ili kuwapa mafunzo walinzi wake.
Jeshi la Polisi lilipiga marufuku vikundi hivyo baada ya kuonekana vinatumika vibaya huku likisisitiza kuwa ndilo lenye mamlaka pekee ya ulinzi na usalama kwa raia wa Tanzania.
Habari zilizolifikia gazeti ili wiki hii na kuthibitishwa na mamlaka mbalimbali za kiusalama serikalini zinadai kuwa Kampuni ya Max Security Solution kutoka Israel inadaiwa kushinda zabuni na tayari imelipwa sh. milioni 450 kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.
Mtandao wa www.max.security.com unaonesha Max Security Solution ni kampuni iliyosajiliwa Isreal na makao makuu yake yapo Tel Aviv na matawi yake yamesambaa maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo Bara la Asia, Afrika na Ulaya.
Kwa mujibu wa mtandao huo kampuni hiyo imejikita zaidi na masuala ya kutoa mafunzo ya ulinzi, ikwemo kufundisha walinzi maalumu kwa viongozi na masuala ya usafirishaji, ambapo kwa hapa nchini inatoa mafunzo hayo na mwalimu wa Israel anayetajwa kwa jina moja la Shaul.
Uchunguzi uliofanywa kutoka vyanzo mbalimbali unaonesha kuwa mafunzo hayo yanafanyika kwa siri katika nyumba iliyoko maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam huku yakihusisha vijana 12 wa Kitanzania (majina yamehifadhiwa kwa sasa) ambao wananolewa kwa umakini mkubwa.
Kwa mujibu habari hizo ni kwamba miongoni mwa mafunzo ambayo vijana hao wanapewa ni pamoja na namna ya kutengeneza uzio wa kumzunguka Lowassa anapokuwa katika halaiki ya watu. Mafunzo mengine ni namna ya kulinda gari lake na pamoja na kutembea naye.
Mafunzo mengine ni namna ya kutembea na kiongozi kwenye msongamano wa watu, namna ya kuwasiliana na kumuokoa pale inapotokea hatari ya ghafla.
Kwa mujibu habari hizo vijana hao 12 wanakaa hoteli moja (jina linahifadhiwa kwa sasa) maeneo ya Mikocheni huku wakilipwa kati ya sh. 500,000 kwa mwezi. Pia, inadaiwa wamepewa maagizo ya kupambana na yeyote kwa gharama yoyote iwapo mazingira yataruhusu.
Pamoja na kwamba haijaelezwa mahali popote iwapo kuna hatari ambayo wanadhani inamkabili mgombea huyo wa urais na kwa nini tahadhari hiyo isitolewe kwa Jeshi la Polisi, ilidaiwa ni kutokana na kambi ya Lowassa kujiapiza kuwa lazima kwenda Ikulu mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari hizo mpango mzima kuleta kampuni hiyo kutoa mafunzo kwa Lowassa umesukwa na mkurugenzi mmoja wa zamani wa Usalama wa Taifa.
Taarifa hizi ni muendelezo wa taarifa za awali zilizowahi kuripotiwa na baadhi ya magazeti na mitandao ya jamii kuwa katika moja ya mikakati ya muda mrefu ya Lowassa kuandaa kundi la vijana na kufanya fujo katika maeneo mbalimbali kwa kisingizio cha kulinda kura Oktoba 25, mwaka huu.
Tayari zipo taarifa kuwa wapo vijana ambao wamepelekwa maeneo mbalimbali nchini na wengine nchi jirani kwa ajili ya mafunzo kama hayo.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu alipoulizwa na gazeti hili jana kama ana taarifa hizo, alisema kutofahamu lolote kuhusu uwepo wa taarifa hizo, lakini aliahidi kuanza kuzifanyia kazi mara moja ili kupata ukweli.
"Nilishaweka wazi kwa vyama vya siasa vyote kutokuwa na vikundi vya kiulinzi na badala yake kama vinahitaji wawasiliane na Jeshi la Polisi kutoa ulinzi," alisema IGP Mangu.Alisisitiza kuwa suala hilo si ombi kwa vile lipo kikatiba, hivyo kwa yeyote atakayekwenda kinyume lazima achukuliwe hatua.
Alisema sheria inayosimamia utegamano wa umma (public order) namba 385 kifungu cha tatu katika sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinakataza muundo wa vikundi vya ulinzi vinavyofanya kazi inayoshabiana na vyombo vya polisi au vya usalama vilivyopo kikatiba nchini.
Ofsa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alipoulizwa kama taarifa hizo zina ukweli ndani yake, alisema habari hizo si geni kwani ni propaganda zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Vyombo vya habari vinavyoshabikia CCM vimeshaandika habari hizo hivyo sioni jipya na sina la kuweza kuzungumzia. Unajua kuna vyombo vinatuandika vibaya na wananchi wanajua hivyo kama kweli una vielelezo nitumie kupitia mtandao nijiridhishe na taarifa hizo," alisema.
Msemaji binafsi wa Lowassa, Aboubakary Liongo alipoulizwa kama anafahamu kuwepo kwa wataalamu wa kijeshi kutoka Israel ili kufundisha kikosi maalumu cha walinzi wa Lowassa, alipokea simu na baada ya mwandishi kujitambulisha na kuelezea kuhusu suala hilo, alikata simu.
Vikosi
Polisi nchini imepiga marufuku vikundi vya ulinzi vya vyama vya kisiasa vyenye mwelekeo wa kijeshi kufanyakazi za ulinzi hadharani kwa madai kuwa vinaingilia majukumu ya Jeshi la Polisi.
Onyo hilo lilitolewa hivi karibuni na Kamishna wa Polisi–Operesheni na Mfunzo, Paul Chagonja wakati akizungumza na waaandishi wa habari Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam.
Chagonja alivitaja vikundi hivyo na vyama vyao kwenye mabano kuwa ni Green Guard (CCM), Red Brigade (Chadema) na Blue Guard (CUF), ambavyo hutumiwa na vyama vya siasa hususan katika mikutano yao.
Agizo la Chagonja limekuja ikiwa ni miezi minne baada ya agizo la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu kupiga marufuku vikundi hivyo vya vyama vya siasa ambavyo vina muonekano na muundo wa vyombo vya usalama, kwani ni kinyume cha katiba na sheria ya nchi.
Alivitaka vyama hivyo kuhakikisha vinafuata muongozo uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa vyama hivyo na kama vikienda kinyume jeshi litapambana navyo.
IGP Mangu aliyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Polisi uliokuwa ukijadili namna ya kuondoa vikundi hivyo pamoja na namna ya kuboresha shughuli za uendeshwaji wa vikundi hivyo.
Alisema vikundi hivyo vipo kinyume cha sheria na kwamba kuendelea kuvimiliki kwa kisingizio chochote ni uvunjifu wa Katiba ya nchi na sheria ya vyama siasa, jambo ambalo polisi haliwezi kulivumilia.
"Polisi imejipanga vizuri kuhakikisha mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa inafanyika katika hali ya utulivu hadi siku ya uchaguzi," alisema Kamishna Chagonja.
Kamishna Chagonja aliwakumbusha wagombea kwa nafasi zao kuwaelimisha wafauasi wao umuhimu wa kuheshimu sheria ili kudumisha amani, usalama na utulivu katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
"Tunatoa tahadhari kwa wananchi pia kuzingatia sheria zinazowaongozwa ikiwamo sheria ya vyama vya uchaguzi na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)," alisema Chagonja.
Akizungumza hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa askari polisi hawatoshi kulinda mkutano wa watu wengi hivyo wataendelea kuwatumia kulinda wanachama wao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema katika chama chao hakuna kikundi kinachoitwa Green Guard kwani hata Katiba ya chama hicho hakina watu kama hao.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa Chama cha CUF, Shaweji Mketo alisisitiza chama chake kuendelea kuwatumia, kwa sababu wapo kikatiba na katiba yao ilipitishwa na Serikali na inatambuliwa na msajili wa vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa Mketo, kauli ya Chagonja ni kutaka wavunje katiba ya chama, kwani maamuzi ya kuwatumia yalipitishwa na mkutano mkuu, “Tutawatumia hiyo ya kutukataza haipo, wapo na katiba ya chama iliweka hilo na msajili wa vyama vya siasa akalipitisha hilo, ina maana hakuona tatizo, ”alisema.
Alifafanua kuwa Red Guard hawajawahi kusababisha matatizo zaidi ya kulinda amani, hivyo hawana sababu ya msingi ya kuacha kuwatumia. Mketo alilalama kuwa kila unapofika uchaguzi kunakuwa na kauli za kukatisha tamaa na kutishwa, wao hawaogopi kwa sababu wamefuata sheria.
Mtikila
Wakati huo huo, Mwenyekiti Taifa wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameibuka na kudai kuwa Lowasa hafai kuwa rais.
Madai hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa kudai mgombea huyo hana sifa za kuwa kiongozi kwani ni fisadi na anatafuta nafasi hiyo kwa fedha na kwamba alipokuwa Waziri wa Ardhi alijimilikisha maeneo kifisadi.
"Ni mwiko kwa Edward Lowassa kupewa kugombea urais kwa sababu si tu alitumia kifisadi uwaziri wa ardhi akajitajirisha na kujipatia maeneo makubwa ya ardhi nchini," alidai na kuongeza kuwa anasaidiwa na watu wa nje kwa lengo la kupata nafasi hiyo.
Mtikila aliongeza kuwa kazi ya rais ni ngumu hivyo inahitaji wenye afya isiyo na tatizo. "ni lazima wagombea wote wachunguzwe kwa makini afya zao," alidai na kuongeza kuwa hitilafu katika afya hudhoofisha uwezo wa kufikiri na kusababisha uamuzi mbovu ambao huleta athari kwa taifa.
Kuhusu Ukawa
Mtikila alidai Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni feki kwani umekiuka matakwa ya umoja halisi.
"Kikwete anapowaumbua Ukawa feki huwa mkweli kwani wanazunguka nchini kote kuwadanganya wananchi, wakijifanya watetezi wa Watanganyika wakati wasaliti," alidai.
"Magufuli si mgombea sahihi kwa taifa hili na Lowassa ndiyo kabisa hawezi hivyo nawaomba Watanzania mkienda kupigakura msichague rais labda mimi kama nitashinda rufani yangu kwani hao waliopo hawana sifa,"
source- jamboleo 17/9/2015
LOWASSA ADAIWA KUKODI MAKOMANDOO WA ISRAEL
Reviewed by habarinamatukioyakijamii.brogspot.com
on
9/18/2015 01:11:00 PM
Rating:
No comments: