KUKUA kwa teknolojia za fedha ambako kumerahisisha ufanisi wa matumizi na utunzaji fedha, kunaonekana kugeuka kuwa balaa kutokana na kuibuka kwa wizi wa fedha zilizohifadhiwa kwenye akaunti za wateja.
Uchunguzi uliofanywa kwa wiki moja sasa umebaini kwamba, katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, ipo hofu kubwa ya wateja wanaotumia huduma za kibenki kuhofia usalama wa fedha zao.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa, hofu hiyo inatokana na tabia iliyoibuka katika siku za hivi karibuni nyakati za sikukuu wezi wa mtandao kutumia mwanya huo kuiba mabilioni ya shilingi kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Fedha zinazotiliwa shaka kuibiwa ni zile zililohifadhiwa katika taasisi za kifedha na fedha zinazohamishwa kwa njia ya M-Pesa, TiGO pesa, Airtel Money huduma nyingine za simu za mikononi.
Hata hivyo, imebainika kuwa kupitia njia ya benki pekee, zipo taarifa kuwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa kampuni zinazotengeneza kadi za ATM kushirikiana na wezi wa mtandao ili kufanikisha zoezi hilo bila waathirika kulipwa fedha zao kwa muda unaofaa.
Hakuna mtumishi yeyote wa taasisi ya kifedha (benki) aliyetaka kunukuliwa kuhusu habari hii ingawa taarifa za awali zinaeleza kuwa, baadhi ya wateja wa benki tofauti nchini wanaohamisha fedha, hutumia njia ya kutembea na fedha mikononi kutokana na kuhofia fedha zao kuingia mikononi mwa wahalifu.
Wengi wa wateja waliona fedha nyingi benki, kwa sasa wamehama kuhifadhi fedha kwa njia hiyo na badala yake wanafanya malipo kwa njia ya M-pesa, TiGO pesa, Airtel Money na njia nyingine katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka baada ya baadhi yao kutapeliwa na wezi kwa njia ya mtandao.
Mmoja wa wateja wa taasisi za kibenki Jijini Dar es Salaam (tunahifadhi jina la taasisi hiyo) amemuambia mwandishi wetu kuwa, tangu mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu, wateja wengi wanaohidhi fedha kwenye taasisi za kifedha, walianza kutoa fedha zao kwa njia mbadala ili kuepuka kuingia mikononi mwa wahalifu wa kimtandao.
Hatima ya fedha za Wateja
Kutokana na wizi huo, hofu ya wateja imeanza huku wengi wao wakihaha na kuhofu juu ya usalama wa fedha zao na iwapo kama zitachukuliwa na wezi hao zitarejeshwa kwao au la.
Gazeti hili mtandao limeelezwa na chanzo chake cha kuaminika kwamba wapo watu wanaotumia mfumo wa kiteknohama kuandaa kadi mpya ili kufanikisha wizi wa ATM hizo au kuuza mfumo wa utengenezaji kadi kwa wajanja ambao huandaa kadi za bandia kwa lengo la kuwasaidia katika wizi huo kwa manufaa binafsi.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, kutoka katika katika taasisi mbalimbali za kibenki, kuna hofu kubwa ambayo imeongezeka katika siku za hivi karibuni juu ya uwezekano wa kutopea kwa fedha nyingi tofauti na zilizowahi kuripotiwa nchini licha ya ukweli kwamba huduma zinazidi kuongezeka na mtandao unazidi kukua na pia wizi wa kwenye mashine za kuchukua fedha (ATM) unafanya watu wengi waamini usalama kwenye simu kuliko benki.
Wimbi la wizi huo limeibuka kwa kasi mwaka 2012 hadi mwaka huu, inakadiriwa Sh700 milioni zimeibwa Benki ya NMB na benki zingine kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2012 na 2013.
Tayari, Jeshi la Polisi katika mikoa mbalimbali nchini kwa kusaidiana na maofisa wa taasisi za kibenki, kwa nyakati tofauti walifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa ambao wanadaiwa kukutwa wakiwa kwenye mpango wa kuendelea kuiba fedha ndani ya mashine za kuchukuliwa fedha (ATM) za benki hizo ikiwemo Benki ya mkoani Mwanza katika siku za hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknologia, hapa nchini kuna kesi zaidi ya 300 za uhalifu wa mitandao ambazo zinachunguzwa na baadhi ziko kwenye hatua ya kufikishwa Mahakamani.
Mmoja wa maofisa wa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknologia (hakupenda jina lake litajwe mtandaoni), ameeleza kwamba kukua kwa kasi kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kumesababisha wizi wa fedha kwa njia ya mtandao, ugaidi, maudhui potofu yanayosababisha mmomonyoko wa maadili, uharibifu wa miundombinu muhimu ya Taifa ikiwamo mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Mkuu wa Chuo cha Teknolojia na Uongozi cha Kilimanjaro ambaye pia ni Mtaalamu wa Ulinzi wa Mitandao, Ezekiel Mpanzo, njia ya kuzuia tatizo hilo ni wataalamu wa hapa nchini kujiunga na vyama vya kuzuia uhalifu wa mitandao duniani kikiwemo cha ‘Ethical Hacking na Sisco’ ili kusaidia kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu wanazotumia wahalifu duniani kote.
Amesema katika mwaka 2010 na robo ya mwaka 2013 Tanzania ilipoteza Sh9.8 bilioni kutokana na wizi huo ambao ulifanywa katika mashine za kutolea fedha maarufu kama ATM.
Mbinu za wizi unavyofanyika
Watumishi kadhaa wa taasisi za kibenki wameithibitishia  kuwa wizi huo hufanyika kwa wahalifu hao kufika katika mashine za kutolea fedha, kwanza huanza kuzima kamera za usalama za eneo husika kwa kuzipulizia rangi maalumu kuzitia ukungu ili kuharibu muonekano wake na kuruhusu wao kuingia eneo hilo bila kuonekana.
Aidha, baada ya kuziharibu kamera za usalama, wamekuwa wakianza kuweka kamera zao za siri kunasa namba za siri za kufungulia akaunti ambazo huzisoma katika kompyuta na kuzinakili katika daftari lao maalumu, kisha kuchukua kadi zao bandia na kuchukua fedha za wateja.
Mathalani, wizi huu mara nyingi hufanyika nyakati za usiku muda ambao huwa hakuna wateja wengi hasa siku za mapumziko. Mbinu nyingine ni wezi kupachika kifaa kama kamera ndogo ya siri inayoweza kurekodi taarifa za mteja kuanzia namba au neno la siri, kiasi cha fedha, jina na kumbukumbu za akaunti ya mteja kwa kuweka kamera juu ya eneo ambako kadi ya ATM huingizwa.
Njia hiyo inatajwa kuwa humponza mteja anapochomeka kadi yake bila kujua mchezo unaoendelea wa mashine hizo kusoma taarifa na baadaye wezi waweze kuandaa mbinu za kuiba kwa njia ya mtandao huku njia nyingine ikielezwa kuwa ni ile ya wafanyakazi wa benki Idara za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) kushirikiana na wezi hao.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, zipo taasisi za kibenki ambazo zimebaini kuwa wapo watumishi wa kampuni zinazotengeneza kadi za ATM wasio waaminifu hushirikiana na wezi wa mtandao kuandaa kadi mpya ili kufanikisha wizi wa ATM.
Hatua za benki kuzuia wizi huo
Uchunguzi wetu umebaini kuwa, hakuna taasisi yeyote ya benki nchini ambayo ipo tayari kuzungumzia suala hili kwasababu wanaogopa kuwashtua wateja wao, lakini habari za ndani zinaeleza wizi huo umekuwa ukigundulika na benki pindi mteja anapolalamika au pale wataalamu wa masuala ya usalama wanapogundua kamera zao zimeharibiwa na hazionyeshi picha katika benki au matawi yenye mashine za ATM.
Ripoti za wizi
Ripoti iliyotolewa na Kampuni ya Kaspersky lab hivi karibuni ilibainisha kuwa genge la wahalifu wa mtandao lilifanikiwa kuiba mamilioni ya Dola za Marekani kutoka kwenye akaunti za wateja wa benki 1,000 katika mataifa 30 kati ya mwaka 2014 na 2015.
Ripoti hiyo ilitoa mfano wa mbinu za genge la Carbanak, linatumia mbinu ya kuambukiza virusi kwenye mashine na kompyuta za benki ikiwamo kamera za CCTV ili kunakili kila kitu kinachoandikwa kwenye komputa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, benki katika mataifa 30 yakiwamo, Russia, Marekani, Ujerumani, China, Ukraine na Kanada yameathirika kwa asilimia kubwa.
Wahalifu mtandao watikisa anga ya wanausalama
Wakati bado mafanikio mbalimbali yakijadiliwa wahalifu mtandao wamegundulika kuja na uhalifu unaotafsiriwa kuwa ni wa kihistoria na uliofanyika kwa ubunifu na umahiri wa hali ya juu ambapo wahalifu mtandao wamefanikiwa kusambaza kirusi aina ya ModPOS kinacho athiri mashine zinazotumika kukamilisha miamala wakati wa manunuzi.
Kirusi cha ModPOS, kimegundulika Nchini Marekani wakati wa sherehe za “Thanks Giving” ambapo watu wengi hufanya manunuzi. Kirusi hicho Kimekua kikifanikisha upotevu mkubwa wa pesa wakati wa miamala.
Mara baada ya ugunduzi huo wa ModPOS, mijadala kupitia mtandao ilianza baina ya wanausalama mitandao ili kuweza kufanikisha mambo makubwa matatu. Moja ni kuweza kugundua chanzo na jinsi ilivyo fanikishwa kuwepo bila kugundulika (Inaaminika kimedumu muda–taarifa ambazo bado zinafatiliwa) Pili, Ilikua ni kutafuta suluhu ya kirusi hicho ili kiweze kuondolewa na Tatu, ni kupanga namna ya kukuza uelewa wa namna ya kujikinga na janga hili la ModPOS.
Hadi sasa bado hapajapatikana suluhu na inahofiwa huwenda kutokana na sherehe za mwisho wa mwaka kirusi hicho kusambaa maeneo mengine huku mataifa yakitakiwa kuchukua tahadhari.
Inakadiriwa kama kitaendelea kutopatiwa suluhu; pesa nyingi zitaishia mikononi mwa wahalifu mtandao na hasara itakayopatikana ni kubwa zaidi kupata kutokea.

USHAURI; kua makini na account zako za bank na tigo,m-pesa,airtell.nk