WAFANYABIASHARA 21 WATUPWA RUMANDE KWA KUDHARAU USAFI
MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Mohamed Utaly amewaweka ndani wafanyabiashara 21 kwa saa 6 kwa kukiuka agizo la Rais la kufanya usafi na kufungua maduka kabla ya muda ulioelekezwa.
Mkuu huyo wa wilaya alichukua hatua hiyo juzi, baada ya wafanyabiashara hao kufungua maduka kabla ya saa nne Sikukuu ya Uhuru ya Desema 9, mwaka huu, huku wananchi wakiendelea na usafi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Mpwapwa na viunga vyake.
Akizungumza na wananchi hao mara baada ya kumaliza kufanya usafi katika viwanja vya Mnara wa Mashujaa, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuzingatia maagizo yatolewayo na viongozi wa Serikali kwa lengo la kuongeza ushirikiano zaidi.
Pia aliwataka kuendeleza utamaduni wa usafi kila baada ya wiki mbili na kuongeza kuwa watatunga sheria ndogo ya utunzaji wa mazingira katika mji wa Mpwapwa na viunga vyake.
Hata hivyo, wananchi walilalamikia halmashauri ya Mpwapwa kwa kushindwa kuweka vituo vya kukusanya taka na kusababisha wananchi kuvamia maeneo ya wazi na kutupa taka hovyo.
Alisema kukosekana kwa gari la usombaji taka katika mji wa Mpwapwa, ndio chanzo kikuu cha mji huo kuendelea kuwa mchafu. Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Mohamed Maje alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya kukosa gari la kusomba taka.
Kuhusu vituo vya kukusanyia taka, aliamuru Ofisa Usafi na Mazingira wa halmashauri hiyo, Emanuel Sallo kukaa na wadau ili kuainisha maeneo hayo.
WAFANYABIASHARA 21 WATUPWA RUMANDE KWA KUDHARAU USAFI
Reviewed by mudy mandai
on
12/12/2015 11:07:00 AM
Rating:
No comments: