RAIS MAGUFULI AWAPATANISHA GWAJIMA NA DK.SLAA
Miezi kadhaa baada ya kutofautiana juu ya ujio wa Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kati ya Mchungaji Josephat Gwajima na Dk. Wilbroad Slaa, Rais John Pombe Magufuli amewezesha wawili hao ‘kupatana’, Risasi Mchanganyiko linaripoti.
Kabla ya tofauti yao, Gwajima ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na Dk. Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, walikuwa ni marafiki chanda na pete.
GWAJIMA JUMAPILI
Katika mahubiri kwa waumini wake kanisani kwake, Ubungo Maji, Dar, Jumapili iliyopita, pamoja na mambo mengine, Mchungaji Gwajima alionesha kufurahishwa kwake na utendaji kazi wa Rais Magufuli ambaye katika mwezi mmoja wa utumishi wake kama kiongozi mkuu wa nchi, amefanya maamuzi mengi magumu na yenye tija kwa jamii.
Mheshimiwa Magufuli hayo unayoyafanya ndiyo Watanzania tumekuwa tukiyapigia kelele miaka yote na tukaonekana wabaya. Tuko sambamba na wewe, tunakuunga mkono, safisha nchi, usilegeze upanga wako wala usijali vitisho vyao. Tunakuombea ushujaa zaidi na roho ya Mungu iwe nawe,” alisema Gwajima mbele ya waumini wake.
DK. SLAA AIBUKA, AMSIFU
Muda mchache baada ya taarifa za Gwajima kuzagaa mitandaoni amemuunga mkono Rais Magufuli, kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forum, Dk. Slaa aliibuka na kumfagilia kiongozi huyo wa kiroho, kwa kitendo chake cha kuubaini ukweli.
“Sina tatizo na Gwajima wala Mtanzania yeyote kumpongeza JPM kwa mafanikio yanayoonekana dhahiri. Akiwa kama kiongozi wa dini, alikuwa na jukumu la kuchunga kondoo. Tulipokuwa tukipinga ufisadi tulijua nini tunafanya, kama leo amegundua kuwa Magufuli ndiyo anafaa, ni jambo jema,” alisema kiongozi huyo wa upinzani mwenye kuheshimika.
JUKWAA LAVAMIWA, WATAKA KUSAMEHEANA
Mara tu baada ya Dk. Slaa kuandika maneno hayo, watu mbalimbali walitoa maoni yao kutaka wawili hao kuweka kando tofauti zao, badala yake wote waungane na kumpa moyo wa kufanya kazi, Rais Magufuli.
“Mimi nadhani huu siyo wakati wa kuendeleza malumbano, wakati ule hawa watu walitofautiana kwa vile kila mmoja alikuwa analipigania taifa. Sasa kama leo wamekutana na wote wanakubaliana na kazi ya Magufuli, ni jambo jema sana. Wasahau yaliyopita, tugange yajayo,” aliandika mtu mmoja anayejiita ChaArusha.
RISASI LAZAMA MTAANI
Baada ya jitihada kubwa kufanyika ili kuwapata viongozi hao wawili kuzungumzia suala hilo, gazeti hili liliamua kuingia mtaani ili kupata maoni ya wananchi juu ya wawili hao wawili, kila mmoja kwa wakati wake kuonekana kukunwa na kazi ya Rais Magufuli.
Japhet Kimaro, aliyejitambulisha kama mfuasi wa Chadema, alisema kama mtu analipenda taifa hili, hawezi kubeza kazi inayofanywa na Rais Magufuli kwa sasa.
“Sikia, mimi nilimwelewa sana Gwajima wakati ule, kwa sababu sijui ungeniambia nini kuhusu Lowassa, lakini baada ya huu mwezi mmoja, hakika nimemkubali Magufuli, Mungu amlinde na simlaumu Gwajima kwa sababu hata mimi nilikuwa kama yeye, sisi hatuichukii CCM, bali tunachukia watu wanaokitumia chama hicho kuiba, kujineemesha.
“Ninajua Dk. Slaa ana uchungu na nchi hii, Gwajima naye anakerwa na maovu ya watu wa serikali, tunachotaka rasilimali zetu zitufaidishe wote, kama anavyotaka rais Magufuli, nawasihi viongozi wangu hawa wamalize tofauti zao, tupige kazi,” alisema msomaji mmoja.
Naye Monalisa Blaise aliyejitambulisha kama Ukawa Kindakindaki, alisema hana tatizo na Magufuli, kwani siku zote wapinzani walitaka mchapakazi wa kuwaondoa mafisadi katika rasilimali za nchi.
“Tokea mwanzo tulijua Magufuli ni mchapakazi, kama alivyokuwa mgombea wetu, lakini tulimtaka zaidi Lowassa kwa sababu ametoka nje ya mfumo, tuliamini mgombea wa CCM ataendeleza ulaji, lakini sasa ni tofauti kabisa, nadhani watu wote wanaoitakia mema nchi yetu ni lazima tuwe pamoja na rais kwa kauli mbiu yake ya hapa kazi tu.”
GWAJIMA, DK. SLAA WAMFUATA PROFESA LIPUMBA
Kitendo cha viongozi hao wawili kusifia utendaji kazi wa kasi wa Rais John Magufuli, ni kama kufuata nyayo za aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye siku chache zilizopita, alikwenda Ikulu jijini Dar kumpongeza kwa mwanzo mzuri wa utawala wake.
Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu cheo chake hicho kabla ya uchaguzi mkuu, alikuwa mpinzani wa kwanza kuelezea waziwazi kufurahishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli ambaye amekuwa akisifiwa kila kukicha kutokana na kasi yake inayowavutia wengi
RAIS MAGUFULI AWAPATANISHA GWAJIMA NA DK.SLAA
Reviewed by habarinamatukioyakijamii.brogspot.com
on
12/09/2015 11:47:00 AM
Rating:
No comments: