MAISHA HALISI YA KASIMU KAYIRA ALIEKUA MTANGAZAJI WA BBC SWAHILI-SEHEMU YA 7
Ahamishiwa kijijini, aacha kazi!
VYEMA kusoma historia za watu waliofanikiwa maishani. Kujua walikotoka na jinsi walivyofanikisha malengo yao, ni kichocheo kikubwa katika kukutia hamasa ya kuzidi kupambana na maisha.
Kassim Abraham Kayira ni miongoni mwa waliogeuza ndoto kuwa uhalisia. Ni mmoja wa watangazaji maarufu ulimwenguni. Amepitia vituo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa. Hapa anasimulia jinsi safari yake ilivyokuwa ngumu kuyafikia mafanikio ya utangazaji aliyonayo.
Yapo matukio mengi aliyowahi kukumbana nayo, ambayo ameyaweka wazi kupitia simulizi hii. Jambo moja na muhimu la wewe kufanya ni kuendelea kufuatilia kila wiki.
Wiki iliyopita, Kayira aliishia kuelezea namna ambavyo aliwekewa zengwe na baadhi ya viongozi baada ya kubaini ufisadi mkubwa wa manunuzi na matumizi ya wabunge wa nchini Rwanda.
Je, nini kilifuata?
SASA ENDELEA…
“Nikwambie kitu mdogo wangu?” ananiuliza Kayira baada ya kuniona nikitafakari kwa kina yale aliyokuwa akinisimulia.
“Naam, kaka,” naitikia na hapohapo namgeukia ili nimsikilize vyema.
“Ukiwa mahali unafanya kazi, lakini misukosuko ikawa mingi, kila siku ukawa mtu wa kuandamwa na wenzako kwa skendo na matatizo mbalimbali ni vyema kabisa kuacha kazi na kuangalia maisha mengine,” anasema Kayira na kunigusa begani huku akinitazama usoni bila kupepesa macho.
“Nilipogundua ufisadi huo, maneno yakawa mengi, ndani na nje ya ofisi, nikaonekana sifai kwa kila mtu, nikahamishiwa kijijini kwenye redio mpya ya Independent, iliyokuwa ikimilikiwa na serikali, nilipoenda kuripoti, sikukaa hata siku moja, nikarudi mjini na kuandika barua ya kuacha kazi,” anasema Kayira na kuongeza;
“Mungu ndiye hutembea na riziki ya mtu, sasa kama huko kazini kila siku ni wewe, hata kama ukifanya jambo dogo tu, zinaibuka tuhuma nzito na kukuzwa kwa maneno makali na yenye kuumiza, nini cha ziada?” anasema Kayira na kuendelea;
“Binadamu hatuna wema hata kidogo mdogo wangu, nimesema hayo nikiwa na maana kubwa sana, ngoja nikusimulie tena,” anasema Kayira lakini kabla hajaendelea, tayari tulikuwa tumewasili Tabata Relini yalipo majengo mengine ya Azam, ambako Kayira alitakiwa kuonana na mhasibu kwa lengo la kukamilisha baadhi ya mahitaji kwa ajili ya safari iliyokuwa ikimkabili siku iliyofuata, safari ya kwenda nchini Uganda.
Haraka sana, Kayira anashuka na kunitaka radhi kwa usumbufu lakini badala ya kumjibu, naishia kukusanya mikono yangu kwa ishara ya kumuonesha kuwa hakuna shida. Ndiyo, ilikuwa lazima nikamilishe mazungumzo yangu na yeye kwa wakati huo.
Haikuchukua muda mrefu akarejea tena ndani ya gari, lakini safari hii hakuwa mweye furaha, uso na rangi ya macho vilikuwa vimebadilika na kuwa nyekundu, tena jasho la hasira likimchuruzika, nikabaini kuwa kuna jambo si jema alikutananalo alikokuwa.
“Vipi kaka?” namuuliza.
“Aaah, sisi Waafrika kufanikiwa ni ngumu sana, kabisa nakuambia mdogo wangu,” anasema huku akifuta jasho jembamba la usoni kwa kitambaa chake.
“Kwa nini unasema hivyo?” namuuliza tena.
“The guy I came to meet is not there, nevertheless he knew that I would be here by this time, he was informed by the boss, uuwiii!”
(Mtu niliyekuja kukutana naye, hayupo, ajabu ni kwamba alijua kwamba nitakuwa hapa kwa muda huu maana alitaarifiwa na bosi, uwiiii!)” Anasema Kayira kwa Kiingereza lakini akiwa na hasira za kukwamishwa na jambo ndiyo maana aliona kama kunieleza kwa Kiswahili angechelewa kuwakilisha hisia zake.
Kufikia hapo, nami naamua kumuonesha Kayira kuwa sikuwa nyuma sana linapokuja suala la kuzungumza lugha ya Kiingereza, naamua kuchangamsha ulimi kidogo.
“You gotta‘ve to pull patience man, hope he‘ll be here in no minute, since he’s aware of thy presence.”
(Unapaswa kuwa mvumilivu ndugu yangu, naamini atakuja muda si mrefu. Anatambua uwepo wako).” Namjibu kwa lugha hiyo, tena kwa kujiamini kupitiliza huku nikirekebisha koo langu kwa kikohozi kikavu.
“Umewahi kuishi nchini Marekani au kuishi na watu wa taifa hilo kwa muda mrefu?” Kayira ananitupia swali ambalo nalikanusha kwa kutingisha kichwa.
“Unazungumza Kiingereza kizuri sana chenye lafudhi ya Kimarekani, hongera sana, nimependa,” anasema Kayira.
“Basi kaka, tuendelee na simulizi yetu,” namrudisha Kayira kwenye mstari wa mazungumzo yetu muhimu.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.
MAISHA HALISI YA KASIMU KAYIRA ALIEKUA MTANGAZAJI WA BBC SWAHILI-SEHEMU YA 7
Reviewed by habarinamatukioyakijamii.brogspot.com
on
12/19/2015 09:20:00 AM
Rating:
No comments: