JE, HAWA HAWAKUFAHAMU UTOROSHWAJI WA MAKONTENA BANDARINI?
Miongoni mwa mambo yanayotikisa duru za vyombo vya habari nchini Tanzania na nje ya nchi ni kuhusu ukwepaji wa kodi kupitia utoroshwaji wa makonte kutoka bandari ya Dar es Salaam.
Hadi sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya makontena 2,500 yalitolewa pasipo kulipiwa kodi stahiki kutoka bandari ya Dar es Salaam kati ya mwaka 2013 hadi 2015.
Bandari ni shirika la Umma ambalo kwa muundo wa Serikali liko chini ya Waziri wa Uchukuzi na kwa taratibu za Bunge linasimamiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo kwa muda huo imekuwa inaongozwa na Mheshimiwa Zitto Kabwe.
Hata hivyo pamoja na hoja binafsi nyingi zilizokuwa zinawasilishwa kwenye meza ya Katibu wa Bunge kuombewa kibali cha kuwasilishwa Bungeni, hakuna kumbukumbu zinazohusu kuombwa kwa hoja binafsi iliyohusu suala hili ambalo ni dhahiri limekuwa linaipotezea Serikali mabilioni ya fedha.
Alipokuwa akihudumu katika serikali ya awamu ya nne kama Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dk. Mwakyembe alijitutumua kukamata makontena yasiyozidi kumi.
Hata hivyo kasi yake ikapungua taratibu na kisha akawa kimya! Aidha, aliyembadili katika nafasi hiyo, Samwel Sitta aliingia kwa nguvu sana lakini hakuweza kugusia eneo hilo kama inavyofanyika sasa.
Haijachukua zaidi ya mwezi mmoja tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani kupata na kuanza kuzifania kazi taarifa kuhusu uozo uliokuwepo katika bandari ya Dar es Salaam. Hili linaacha maswali mengi yanayohitaji majibu.
1.Je, ilikuwaje watoa taarifa hizi walishindwa kuzifikisha taarifa hizi kwa wasimamizi wa bandari na mashirika ya umma wa wakati huo wakiwemo mawaziri Dk. Harrison Mwakyembe, Samwel Sitta na Kabwe Zitto (Mwenyekiti wa PAC)?
2.Je, inawezekana kuwa walikuwa na taarifa lakini nao walinyamazishwa?
3.Je, kama walinyamazishwa ilikuwa kwa maslahi ya nani?
4.Je, ni mfumo gani ufuatwe ili PAC iweze kuwawakilisha wananchi pasipo shaka katika kuisimamia Serikali?
5.Je, si wakati muafaka kwa waheshimiwa hawa na wale wanaoendelea kuwemo katika Bunge la awamu hii ya uongozi, kujitokeza kueleza wanachokifahamu kuhusu sakata hili na kilichowanyamazisha ili waweze kuaminika tena?
JE, HAWA HAWAKUFAHAMU UTOROSHWAJI WA MAKONTENA BANDARINI?
Reviewed by mudy mandai
on
12/13/2015 08:26:00 AM
Rating:
No comments: